Soma Biblia Kila Siku Aprili/2022Mfano
Msalabani Yesu alisema maneno saba mbalimbali, k.mf. hili la m.34:Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Yesu aliwaombea hao askari waliomsulibisha! Aliona ni watu wasiomjua Mungu, ni watu ambao wamepotea. Hakuwatakia mabaya bali mema! Je, huu si upendo wa ajabu? Ni upendo utokao juu, upendo uliojaa moyoni mwa Mungu. Na Yesu anatuita sisi wafuasi wake tuwe na upendo kama huu kwa adui zetu! Je, inawezekana kweli? Ndiyo, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu! Tuone zaidi jinsi Neno la Mungu linavyofundisha kuhusu uhusiano kati ya upendo wa Mungu na msamaha:Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu(Mt 5:43-48).na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi(Rum 5:5).Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake(Mdo 7:54-60).
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Soma Biblia Kila Siku Aprili/2022 ni mpango wa kusoma Biblia sehemu kwa sehemu kila siku kwa mwezi wa Aprili pamoja na maelezo mafupi yatakayokusaidia kuelewa kwa urahisi na kuendelea kutafakari neno la Mungu ulilosoma kwa siku husika. Katika mpango huu utasoma zaidi katika kitabu cha Luka na Tito. Karibu kujiunga na mpango huu na usome bure.
More
Tungependa kuwashukuru Soma Biblia kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea: http://www.somabblia.or.tz/