Soma Biblia Kila Siku Septemba 2021Mfano
Mpaka sasa halijaandikwa neno lolote baya juu ya Daudi. Kama ingaliendelea hivyo tungalijiuliza: Je, Daudi alikuwa mtakatifu kabisa? Lakini katika mlango wa 11 na 12 kuanguka kwa Daudi kumeelezwa wazi kabisa, tena ni aibu kubwa! Na kufuatana na sheria yao, adhabu yake ilitakiwa kuwa kifo (12:5, Daudi akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa. Law 20:10, Mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa. Kum 22:22, Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli). Ila hata hapo Daudi alionekana kuwa mcha Mungu, maana alipojulishwa dhambi zake hakujaribu kuficha! Jinsi Daudi alivyoanguka katika uzinzi ni mfano wa maneno ya Yak 1:12-16, Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Soma Biblia Kila Siku Septemba 2021 ni mpango mzuri wa kusoma Biblia kila siku sehemu kwa sehemu hasa katika kitabu cha Wakolosai, 2 Samweli na Ufunuo. Mpango huu una maelezo mafupi yatakayokusaidia kuelewa zaidi Neno la Mungu. Karibu kujiunga na mpango huu
More
Tungependa kuishukuru Soma Biblia kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea: http://www.somabiblia.or.tz/