Soma Biblia Kila Siku 11Mfano
Waisraeli kumkataa Kristo kulifanya Mataifa yabarikiwe na utajiri wa Kristo! Tafakari Paulo na Barnaba wanavyosema katika Matendo 13:44-47, Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Kwa hiyo katika Rum 11:12 Paulo anauliza, Ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao? (m.12). Ndipo anatufunulia siri ya mpango wa Mungu kwamba kweli siku moja wengi wao wataokoka. Katika m.25-27 anaandika: Ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.Kwa maneno haya tunajulishwa zaidi maana ya utimilifu katika 11:12. Hayo yatatokea baada ya Injili kuenezwa kwa Mataifa yote, na ulimwengu utabarikiwa sana kwa kuokoka kwao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?(11:15)! Ndivyo Mungu atakavyotimiza ahadi yake kwa Ibrahimu katika Mwanzo 12:3: Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Soma Biblia Kila Siku 11 ni mpango mzuri wa kusoma Biblia sehemu kwa sehemu na kupata maelezo mafupi ya kukusaidia kuendelea kutafakari na kuelewa Neno la Mungu. Mpango huu unagusa zaidi Warumi na 1 Samweli.
More
Tunapenda kumshukuru Soma Biblia kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea: http://www.somabiblia.or.tz