BibleProject | Safari ya Kujifunza Kutoka Luka Na MatendoMfano
Ufalme wa Yesu ni habari njema kwa wanaoteseka, na pia ni habari njema kwa wote wanaofahamu kwamba wanamhitaji Mungu. Ili kufafanua hili, Luka anatueleza jinsi Yesu alihudhuria karamu za jioni, karamu ambazo zilikuwa na wagonjwa na maskini waliopokea msamaha, uponyaji na ukarimu wake. Kwa upande mwingine, Yesu pia anahudhuria karamu za jioni ambako kulikuwa na viongozi wa dini waliokataa mafundisho yake na kukosoa mbinu zake. Hawafahamu Ufalme wa Mungu unahusu nini, hivyo anawaeleza fumbo. Alisimulia kama ifuatavyo.
Kulikuwepo na baba aliyekuwa na wana wawili. Mwana wa kwanza ni mwadilifu na anamheshimu babake, lakini yule mdogo amepotoka. Anachukua urithi wake mapema, anakwenda nchi ya mbali na kuutumia kwa uasherati na anasa. Baadaye njaa kuu inaingia nchi aliyokuwa akiishi na mali yake inakwisha, naye anapata kazi ya kuwalisha nguruwe. Siku moja anaona njaa kali mpaka yuko tayari kula chakula cha nguruwe, ndipo akawaza kuwa maisha yake yangekuwa bora hata angelikuwa mtumishi wa babake. Hivyo anaondoka na kurejea nyumbani, huku akifanya mazoezi ya jinsi atakavyoomba msamaha. Anapokuwa angali mbali, baba yake anamwona na anajawa na furaha. Mwanaye yu hai! Hajaangamizwa na njaa! Baba anamwendea mbio na anamkumbatia na kumbusu. Mwana anaanza kwa kusema, “Baba, sistahili kuitwa mwanao. Nifanye mmoja wa watumishi wako...” Lakini kabla hajamaliza kunena, baba anawatuma watumishi wake wamletee mwanawe vazi lililo bora wamvike, viatu vipya na pete nzuri. Wanapaswa kuandaa karamu kuu kwa sababu ni wakati wa kusherehekea kurejea kwa mwana. Karamu inapoanza, yule ndugu mkubwa anarejea kutoka kufanya kazi ngumu na anapofika anagundua kuwa muziki na vyakula vimeandaliwa kwa ajili ya ndugu yake mpotevu. Anakasirika na anakataa kuingia kwenye karamu. Baba anamkuta mwanawe wa kwanza nje na anamwambia, “mwanangu, tayari wewe ni sehemu ya familia yetu. Vyote nilivyo navyo ni vyako. Lakini ilitupasa tusherehekee kurejea kwa ndugu yako. Alikuwa mpotevu lakini sasa amerejea. Alikuwa amekufa, lakini sasa yu hai.”
Kwenye simulizi hii, Yesu anawalinganisha viongozi wa kidini na yule mwana wa kwanza. Yesu anaona jinsi viongozi wa dini wanavyoghadhabishwa na kitendo chake cha kuwapokea wenye dhambi, lakini Yesu angependa viongozi hawa wawachukulie wenye dhambi jinsi yeye anavyowachukulia. Wenye dhambi wanarejea kwa baba yao. Wana uzima! Wema wa Mungu unawatosha watu wote. Vyote alivyo navyo ni vya wale anaowaita wana wake.
Kuhusu Mpango huu
Safari ya Kujifunza Kutoka Luka Na Matendo huwahimiza watu, vikundi vidogo, na familia kusoma vitabu vya Luka na Matendo ya Mitume kwa siku 40. Mpango huu unajumuisha video zilizohuishwa na mihtasari ili kuwasaidia washiriki kukutana na Yesu. Na kujifunza kutoka kwenye usanifu mwema wa kifasihi wa Luka na mtiririko wa mawazo.
More
Tungependa kuwashukuru BibleProject na YouVersion kwa kutupa somo hili. Kwa taarifa za ziada, tafadhalo tembelea: www.bibleproject.com na www.youversion.com