BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 2 - Matendo ya MitumePrøve
Luka anatuambia jinsi Paulo anavyopigwa mara kwa mara, kufungwa gerezani, au hata kuburutwa kutoka kwenye miji mbalimbali kwa kutangaza kuwa Yesu ndiye masihi Mfalme wa Wayahudi na wa ulimwengu wote. Paulo anapofika Korinto, anatarajia kuteswa tena. Lakini Yesu anamfariji Paulo na kukutana naye katika maono usiku mmoja akisema, “Usiogope, endelea kuzungumza na usinyamaze. Niko na wewe. Hakuna atakayekushambulia wala kukuumiza, kwa sababu nina wengi katika jiji hili.” Na kwa hakika, Paulo anaweza kuishi katika jiji kwa mwaka mzima na nusu, akifundisha kutoka kwenye Maandiko na kuhubiri habari za Yesu. Na watu wanapojaribu kumshambulia Paulo, kama Yesu alivyosema tu, hawafanikiwi. Na kiongozi aliyejaribu kumuumiza Paulo anashambuliwa yeye badala ya Paulo. Paulo hafukuzwi kutoka Korinto, lakini katika wakati unaofaa, anaondoka jijini na marafiki wapya ili kuwatia nguvu wanafunzi waliokuwa wanaishi Kaisaria, Antiokia, Galatia, Frigia na Efeso.
Huko Efeso, Paulo anawatambulisha wafuasi wapya wa Yesu juu ya karama ya Roho Mtakatifu, na anafundisha kwa miaka kadhaa, akieneza habari njema kumhusu Yesu kwa wote wanaoishi Asia. Huduma hiyo inastawi watu wengi wanavyoponywa kimiujiza na kuachiliwa huru, wengi kiasi kwamba mpaka uchumi wa jiji unaanza kubadilika watu wanapoacha uchawi na kuacha sanamu zao ili kumfuata Yesu. Wafanyabiashara wanaofaidika kutoka kwenye ibada ya sanamu wanakasirika na kuanza kuchochea umati wa watu kumtetea mungu wao wa kike na kupigana na wale wanaosafiri na Paulo. Jiji linakanganyika, na ghasia hiyo inaendelea hadi karani wa mji anapozungumza.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
• Linganisha maneno ya Yesu kwa Paulo katika Matendo ya Mitume 18:9-10 na maneno ya Yesu katika Mathayo 28:19-20. Unatambua nini? Pia tazama Maneno ya Mungu kwa Israeli kupitia kwa nabii wake katika Isaya 41:10. Unatambua nini? Maneno ya Yesu yanakutia moyo au kukupatia changamoto vipi leo?
• Unapozingatia maneno ya Yesu kwa Paulo katika mistari 9-10, unafikiri inamaanisha nini kuwa Yesu ana watu wengi jijini? Je, wewe ni mmoja wa watu wa Yesu katika jiji lako?
• Warumi waliamini kuwa miungu ingeweza kulinda na kuleta mafanikio katika jiji lao, kwa hivyo waliabudu sanamu nyingi. Sanamu inaweza kuwa kitu chochote ambacho mtu anategemea kando na Yesu kwa ajili ya usalama au faraja. Baadhi ya sanamu katika jiji lako ni zipi? Ikiwa watu wengi katika mji wako wangeacha hizi sanamu na kumwabudu Yesu, hilo lingeathiri uchumi vipi?
• Ruhusu mawazo yako yachochee maombi. Dhihirisha shukrani zako kwa Yesu. Mwambie unakotaka akuhakikishie na jinsi unavyotaka kuona ujumbe wake wenye nguvu ukibadilisha jiji lako. Muombe ujasiri, ili uweze kujiunga na mipango yake leo.
Om denne planen
BibleProject ilibuni Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarajio Sehemu ya 2 ili kuwatia watu moyo, vikundi vidogo, na familia mbali mbali waweze kusoma Matendo ya Mitume kwa siku 20. Mpango huu unajumuisha video za katuni, mihtasari yenye mawazo yanayojenga, na maswali ya tafakari ili kuwasaidia washiriki kukutana na Yesu na kuzama kwenye ubunifu wa fasihi wa mwandishi na kuelewa na kujifunza kutoka kwenye mtiririko wa mawazo yake.
More