BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaPrøve
Luka anawahoji mashahidi wengi wa mwanzo zaidi waliofahamu maisha ya Yesu kisha anaandika simulizi yake kuhusu Injili. SImulizi inaanzia kwenye milima ya Yerusalemu ambako manabii wa kale wa Israeli walitabiri kuwa Mungu mwenyewe atakuja siku moja kuanzisha Ufalme wake kote duniani.
Siku moja katika hekalu la Yerusalemu, kuhani aitwaye Zakaria anaendelea na kazi za ukuhani na ghafla anaona maono yaliyomshtua. Malaika anamtokea na kumweleza kuwa yeye na mkewe watapata mtoto wa kiume. Huu ni ujumbe wa kustaajabisha kwani Luka anatueleza kwamba Zakaria na mkewe ni wazee sana na hawajawahi kupata watoto. Kwa maelezo haya, Luka anatengeza mlinganisho wa simulizi yao na simulizi ya Abrahamu na Sara, mababu wakuu wa Israeli. Wao pia walikuwa wazee sana na hawakuweza kupata watoto hadi pale Mungu kwa muujiza aliwapa mwana, Isaka, ambaye kupitia kwake simulizi nzima ya Israeli ilianza. Hivyo hapa Luka anadokeza kuwa Mungu yu karibu kutenda muujiza wenye dhumuni kubwa kwa mara nyingine tena. Malaika anamwambia Zakaria amwite mwanawe Yohana. Anamweleza kwamba mwanawe ndiye aliyetabiriwa na manabii wa kale wa Israeli waliposema kuwa atakuja yule ambaye ataiandaa Israeli kukutana na Mungu wao atakapofika kutawala Yerusalemu. Zakaria haamini maneno ya malaika, na anafanywa kuwa bubu hadi Yohana alipozaliwa.
Malaika huyo huyo pia anamtokea bikira aitwaye Mariamu na habari kama hiyo ya kushangaza. Yeye pia kupitia muujiza atapata mtoto aliyetabiriwa na manabii wa Israeli. Malaika anamwambia amwite mwanawe Yesu na kuwa atakuwa mfalme kama Daudi ila yeye atatawala watu wa Mungu milele. Anafahamu kuwa Mungu atajivika ubinadamu kwenye tumbo lake na kwamba atamzaa Masihi. Na ghafla ghafla tu, Mariamu anabadilika kutoka kuwa msichana wa kawaida tu, na kufanywa kuwa mama wa mfalme atakayekuja. Anastaajabu kisha anaanza kuimba kuhusu jinsi kuinuliwa kwa hadhi yake katika jamii kunaashiria mwamko mkuu zaidi unaokuja. Kupitia mwanawe, Mungu atawashusha watawala kutoka kwenye viti vyao vya enzi na kuwainua masikini na walio wanyenyekevu. Atapindua taratibu za ulimwengu mzima.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
•Linganisha yaliyowafanyikia Zakaria na Elisabeti na yale yaliyowafanyikia Ibrahimu na Sara. Je, ni kipi kiliwafanya wanandoa hawa kutoamini na kusadiki ahadi za Mungu? Soma Luka 1:5-25 na Mwanzo 15:1-6, 16:1-4, 17:15-22, 18:9-15, 21:1-7.
•Je, Mariamu na Zakaria wanachukulia vipi ujumbe wa kustaajabisha unaoletwa na malaika? Tambua tofauti kati ya maswali wanayomuuliza malaika. Zakaria anataka hakikisho kuwa yaliyosemwa yatatimia, naye Mariamu anataka kujua yatatimia vipi. Mmoja ana shaka na mwingine ana shauku. Je, huwa unapokea vipi habari za Ufalme wa Mungu?
•Linganisha wimbo wa Mariamu (Luka 1:46-55) na wimbo wa Hana (1 Samweli 2:1-10). Unatambua nini? Je, wimbo wa Mariamu na ule wa Hana unaonyesha vipi jinsi Ufalme wa Mungu ni wa kipekee?
•Kusoma na kutafakari kwako kukuchochee kuomba. Zungumza na Mungu kuhusu kilichostaajabisha na jinsi unavyokubaliana na ujumbe wake. Kiri mashaka yako na umwombe unachohitaji.
Skriften
Om denne planen
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More