BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaPrøve
Kwenye sehemu hii inayofuata, Luka anaangazia matukio ya baadaye. Yohana sasa ndiye nabii anayeongoza huduma ya toba kwenye Mto Yordani, na umati wa watu unakuja kubatizwa––maskini, matajiri, watoza ushuru na hata askari. Watu hawa wote wanajitolea kuishi maisha mapya. Hapo zamani, wana wa Israeli walirithi nchi yao kwa kuvuka mto huu huu na Mungu aliwapa jukumu. Waliitwa kumtumikia yeye pekee, kuwapenda jirani zao na kutenda haki kwa pamoja. Tunafahamu kutoka kwenye simulizi za Agano la Kale kwamba hawakutii amri hii mara kwa sehemu kubwa, hivyo Yohana anaiita Israeli kuanza upya––kubatizwa kwenye Mto Yordani ili kusalimu na kujikita upya kwa Mungu wao. Ubatizo huu utawaanda kwa kile Mungu anaenda kutenda.
Ni hapa Mto Yordani ambapo Yesu anajitokeza tayari kuanza kazi yake ya Ufalme. Yesu anabatizwa na Yohana, na anapotoka majini, mbingu inafunguka na sauti inasikika ikisema, “Wewe ni mwanangu ninayempenda, nimependezwa sana nawe.” Maneno ya Mungu hapa yanafanana na Maandiko ya Kiebrania. Mstari huu wa kwanza unapatikana kwenye kitabu cha Zaburi sura ya 2, ambapo Mungu aliahidi kuwa mfalme atakuja kutawala Yerusalemu ili kukabiliana na uovu katika mataifa. Mstari unaofuata unapatikana kwenye kitabu cha nabii Isaya, na unamrejelea Masihi atakayefanyika mtumishi na atateswa na kufa kwa niaba ya Israeli.
Baada ya haya, Luka anafuatilia jinsi uzao wa Yesu umetoka kwa Daudi (mfalme wa Israeli), Abrahamu (baba wa Israeli), Adamu (baba wa wanadamu) na kwa Mungu (muumba vyote). Kwa hili, Luka anatusaidia kumwona Yesu kama Mfalme masihi aliyetoka kwa Mungu kukomboa wanadamu wote na sio Israeli peke yake.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
•Linganisha Luka 3:21-22 na maneno ya Mungu katika Isaya 42:1-4 na Zaburi 2:7-9. Unagundua nini?
•Soma unabii uliozungumzia sifa na kazi ya Yohana Mbatizaji (Isaya 40:3-5, Malaki 4:5). Linganisha vifungu hivi na ujumbe wa Yohana katika kitabu cha Luka 3:7-14. Unatambua nini?
•Je, Yohana Mbatizaji na umati walimpokea vipi Mfalme Yesu alipojitokeza hadharani? Je, unampokea vipi leo?
•Yesu ndiye Mfalme masihi, anayetupa mwanzo mpya. Kwake yeye tunaweza kukubalika mbele za Mungu. Tenga muda umwombe. Mshukuru, mweleze taabu zako na umwombe kile unachohitaji.
Om denne planen
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More