Yobu 21:1-16
Yobu 21:1-16 BHN
Kisha Yobu akajibu: “Sikilizeni kwa makini maneno yangu; na hiyo iwe ndiyo faraja yenu. Nivumilieni, nami nitasema, na nikisha sema endeleeni kunidhihaki. Je, mimi namlalamikia binadamu? Ya nini basi, nikose uvumilivu? Niangalieni, nanyi mshangae, fumbeni mdomo kwa mkono. Nikifikiri yaliyonipata nafadhaika nafa ganzi mwilini kwa hofu. Kwa nini basi waovu wanaishi bado? Mbona nguvu zao zaongezeka hata uzeeni? Huwaona watoto wao wakifanikiwa; na wazawa wao wakipata nguvu. Kwao kila kitu ni salama bila hofu; wala kiboko cha Mungu hakiwafikii. Naam, ng'ombe wao wote huongezeka, huzaa bila matatizo yoyote. Watoto wao wachanga huwatembeza kama kundi; na watoto wao hucheza ngoma; hucheza muziki wa ngoma na vinubi, na kufurahia sauti ya filimbi. Huishi maisha ya fanaka kisha hushuka kwa amani kuzimu. Humwambia Mungu, ‘Usitusumbue! Hatutaki kujua matakwa yako. Mungu Mwenye Nguvu ni nini hata tumtumikie? Tunapata faida gani tukimwomba dua?’ Kufanikiwa kwao si kuko mikononi mwao, wakiwa wamemweka Mungu mbali na mipango yao?