Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayu 21:1-16

Ayu 21:1-16 SUV

Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Yasikizeni sana maneno yangu; Jambo hili na liwe faraja yenu. Niacheni, nami pia nitanena; Tena nikiisha nena, zidini kudhihaki. Mimi, je! Mashitaka yangu yamhusu mwanadamu? Nami kwa nini nisikose kusubiri? Niangalieni, mkastaajabu, Mkaweke mkono kinywani. Hata nikumbukapo nahuzunika, Na utisho wanishika mwilini mwangu. Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu? Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao. Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi. Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng’ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba. Huwatoa kama kundi watoto wao. Na watoto wao hucheza. Huimba kwa matari na kwa kinubi, Na kuifurahia sauti ya filimbi. Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula. Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako. Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba? Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao; Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.