Ayubu 21:1-16
Ayubu 21:1-16 NEN
Ndipo Ayubu akajibu: “Yasikilizeni maneno yangu kwa makini; hii na iwe faraja mnayonipa mimi. Nivumilieni ninapozungumza, nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki. “Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu? Kwa nini nisikose subira? Niangalieni mkastaajabu; mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu. Ninapowaza juu ya hili, ninaogopa, nao mwili wangu unatetemeka. Kwa nini waovu wanaendelea kuishi, wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu? Huwaona watoto wao wakithibitika wakiwa wamewazunguka, wazao wao mbele za macho yao. Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu; fimbo ya Mungu haiko juu yao. Madume yao ya ngʼombe huvyaza bila kushindwa kamwe; ngʼombe wao huzaa wala hawaharibu mimba. Huwatoa watoto wao nje kama kundi; wadogo wao huchezacheza. Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi, nao huifurahia sauti ya filimbi. Huitumia miaka yao katika mafanikio nao hushuka kaburini kwa amani. Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’ Hatuna haja ya kufahamu njia zako. Mwenyezi ni nani hata tumtumikie? Tutapata faida gani kumwomba? Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe, hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.