Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 21

21
Jibu la Yobu
1Kisha Yobu akajibu:
2“Sikilizeni kwa makini maneno yangu;
na hiyo iwe ndiyo faraja yenu.
3Nivumilieni, nami nitasema,
na nikisha sema endeleeni kunidhihaki.
4Je, mimi namlalamikia binadamu?
Ya nini basi, nikose uvumilivu?
5Niangalieni, nanyi mshangae,
fumbeni mdomo kwa mkono.
6Nikifikiri yaliyonipata nafadhaika
nafa ganzi mwilini kwa hofu.
7Kwa nini basi waovu wanaishi bado?
Mbona nguvu zao zaongezeka hata uzeeni?
8Huwaona watoto wao wakifanikiwa;
na wazawa wao wakipata nguvu.
9Kwao kila kitu ni salama bila hofu;
wala kiboko cha Mungu hakiwafikii.
10Naam, ng'ombe wao wote huongezeka,
huzaa bila matatizo yoyote.
11Watoto wao wachanga huwatembeza kama kundi;
na watoto wao hucheza ngoma;
12hucheza muziki wa ngoma na vinubi,
na kufurahia sauti ya filimbi.
13Huishi maisha ya fanaka
kisha hushuka kwa amani kuzimu.
14Humwambia Mungu, ‘Usitusumbue!
Hatutaki kujua matakwa yako.
15Mungu Mwenye Nguvu ni nini hata tumtumikie?
Tunapata faida gani tukimwomba dua?’
16Kufanikiwa kwao si kuko mikononi mwao,
wakiwa wamemweka Mungu mbali na mipango yao?#21:16 tafsiri inayolingana na Septuaginta. Kiebrania: Shauri la waovu liko mbali nami.
17“Mara ngapi umepata kuona mwanga wa maisha ya mwovu umezimwa,
wakapata kukumbwa na maafa,
au Mungu amewahi kuwaangamiza kwa hasira yake?
18Hata hivyo, na wapeperushwe kama majani makavu,
wawe kama makapi yanayochukuliwa na dhoruba!
19“Nyinyi mwasema, ‘Mungu amewawekea watoto wao
adhabu ya watu hao waovu.’
Kwa nini hawalipizi wao wenyewe, wapate kutambua!
20Waone wao wenyewe wakiangamia;
waone wenyewe ghadhabu ya Mungu mwenye nguvu.
21Maana wakifa watajali nini juu ya wazawa wao,
wakati siku zao zitakapokuwa zimefika mwisho?
22Je, binadamu aweza kumfunza Mungu maarifa,
Mungu ambaye huwahukumu wakazi wa mbinguni?
23“Mtu hufa katika kilele cha ufanisi wake,
akiwa katika raha mustarehe na salama;
24amejaa mafuta tele mwilini,
na mifupa yake ikiwa bado na nguvu.
25Mwingine hufa na huzuni kubwa moyoni,
akiwa hajawahi kuonja lolote jema.
26Hata hivyo, wote hufa na kuzikwa,
wote hufunikwa na mabuu.
27“Sikilizeni! Mimi nayajua mawazo yenu yote,
na mipango yenu ya kunidharau.
28Eti mwauliza, ‘Iko wapi nyumba ya mkuu?
Iko wapi nyumba alimoishi mwovu?’
29“Je, hamjawauliza wapita njia,
mkakubaliana na ripoti yao?
30Mwovu husalimishwa siku ya maafa,
huokolewa siku ya ghadhabu!
31Ni nani atakayemshutumu mtu mwovu,
au atakayemlipa kwa yote aliyotenda?
32Anapochukuliwa kupelekwa kaburini,
kaburi lake huwekewa ulinzi.
33Watu wengi humfuata nyuma
na wengine wengi sana humtangulia.
Anapozikwa, udongo huteremshwa taratibu.
34Mtawezaje basi, kunifariji kwa maneno matupu?
majibu yenu hayana chochote ila uongo.”

Iliyochaguliwa sasa

Yobu 21: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia