Zaburi 59:10-17
Zaburi 59:10-17 SRUV
Mungu wa fadhili zangu atanitangulia, Mungu atanijalia kutazama kwa ushindi juu ya adui zangu. Usiwaue, watu wangu wasije wakasahau; Uwatawanye kwa uweza wako, Na kuwaangamiza, Ee Bwana, ngao yetu. Kwa dhambi ya kinywa chao, Na kwa neno la midomo yao, Wanaswe kwa kiburi chao, Kwa ajili ya kulaani na uongo wasemao. Uwakomeshe kwa hasira, Uwakomeshe watoweke, Wajue ya kuwa Mungu atawala katika Yakobo, Na hata miisho ya dunia. Wakati wa jioni hurudi, wakilia kama mbwa, Na kuzungukazunguka mjini. Wanatangatanga wakitafuta chakula; Na kunung'unika wasiposhiba. Nami nitaimba juu ya nguvu zako, Nitaimba kwa furaha juu ya fadhili zako asubuhi. Maana umekuwa ngome yangu, na kimbilio wakati wa mateso yangu. Ee nguvu zangu, nitakuimbia sifa, Maana Ewe Mungu ndiwe ngome yangu, Mungu wa fadhili zangu.