BibleProject | Safari ya Kujifunza Kutoka Luka Na MatendoSample
Kwenye sehemu hii inayofuata, Luka anaangazia matukio ya baadaye. Yohana sasa ndiye nabii anayeongoza huduma ya toba kwenye Mto Yordani, na umati wa watu unakuja kubatizwa––maskini, matajiri, watoza ushuru na hata askari. Watu hawa wote wanajitolea kwa maisha mapya. Zamani, wana wa Israeli walikuja kurithi nchi yao kwa kuvuka mto huu huu na Mungu aliwapa jukumu. Waliitwa kumtumikia yeye pekee, kuwapenda jirani zao na kutenda haki kwa pamoja. Tunafahamu kutokana na simulizi katika Agano la Kale kwamba hawakutii amri hii mara kwa mara, hivyo Yohana anaita Israeli kuanza upya––kubatizwa kwenye Mto Yordani ili kujikabidhi upya kwa Mungu wao. Ubatizo huu wa ondoleo la dhambi utawaanda kwa kile Mungu anaenda kutenda.
Ni hapa Mto Yordani ambapo Yesu anajitokeza tayari kuanza kazi yake ya Ufalme. Yesu anabatizwa na Yohana, na anapotoka majini, mbingu inafunguka na sauti inasikika ikisema, “Wewe ni mwanangu ninayempenda, nimependezwa sana nawe.” Maneno ya Mungu hapa yanahusiana na Maandiko ya Kiebrania. Mstari huu wa kwanza unapatikana kwenye kitabu cha Zaburi sura ya 2, ambapo Mungu aliahidi kuwa mfalme atakuja kutawala Yerusalemu ili kukabiliana na uovu katika mataifa. Mstari unaofuata unapatikana kwenye kitabu cha nabii Isaya, na unamrejelea Masihi ambaye atafanyika mtumishi na atateswa na kufa kwa niaba ya Israeli.
Baada ya haya, Luka anafuatilia jinsi uzao wa Yesu umetoka kwa Daudi (mfalme wa Israeli), Ibrahimu (baba wa Israeli), Adamu (baba wa wanadamu) na kwa Mungu (muumba vyote). Kwa hili, Luka anatusaidia kumwona Yesu kama Mfalme masihi aliyetoka kwa Mungu kukomboa sio Israeli tu bali wanadamu wote.
About this Plan
Safari ya Kujifunza Kutoka Luka Na Matendo huwahimiza watu, vikundi vidogo, na familia kusoma vitabu vya Luka na Matendo ya Mitume kwa siku 40. Mpango huu unajumuisha video zilizohuishwa na mihtasari ili kuwasaidia washiriki kukutana na Yesu. Na kujifunza kutoka kwenye usanifu mwema wa kifasihi wa Luka na mtiririko wa mawazo.
More