Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 18:21-50

Zaburi 18:21-50 BHN

Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia; nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu; yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia. Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu; mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu; lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wenye majivuno huwaporomosha. Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Kwa msaada wako nakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta. Huyu Mungu matendo yake hayana dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama. Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu? Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu? Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande; ndiye anayeifanya salama njia yangu. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele. Hunifunza kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. Umenipa ngao yako ya kuniokoa; mkono wako wa kulia umenitegemeza; wema wako umenifanikisha. Umenirahisishia njia yangu; wala miguu yangu haikuteleza. Niliwafuatia adui zangu na kuwakamata; sikurudi nyuma mpaka nimewaangamiza. Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha maadui chini yangu. Uliwafanya maadui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walipiga yowe lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi-Mungu lakini hakuwajibu. Niliwatwanga wakawa kama vumbi inayopeperushwa na upepo; niliwakanyaga kama tope la njiani. Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu, ukanifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wa usalama wangu; atukuzwe Mungu wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi; na kuyashinda mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka kwa maadui zangu, akanikuza juu ya wapinzani wangu, na kunisalimisha mbali na watu wakatili. Kwa hiyo nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo mteule wake, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.

Soma Zaburi 18

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 18:21-50