Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 18:21-50

Zaburi 18:21-50 SRUV

Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikubandukana nazo. Nami nilikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu. Ndipo BWANA akanilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi. Maana Wewe wawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili. Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; BWANA Mungu wangu aniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya BWANA imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu ila BWANA? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu? Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Anaifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kulia umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezipanulia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza. Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hadi wakomeshwe. Nitawapigapiga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu. Nawe umenipa nguvu za vita, Hunitiishia chini yangu walionishambulia. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali. Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita BWANA lakini hakuwajibu, Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani. Umeniokoa kutoka kwa mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Mara tu waliposikia habari zangu, wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; Ndiye Mungu anilipizaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu mjeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na wazawa wake hata milele.

Soma Zaburi 18

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 18:21-50

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha