Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 18:21-50

Zaburi 18:21-50 NEN

Kwa maana nimezishika njia za BWANA; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu. Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake. Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi. BWANA amenilipa sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake. Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia. Kwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi. Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini huwashusha wenye kiburi. Wewe, Ee BWANA, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka; Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga. Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta. Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la BWANA halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake. Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya BWANA? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu? Mungu ndiye anivikaye nguvu na kufanya njia yangu kuwa kamilifu. Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu. Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba. Hunipa ngao yako ya ushindi, nao mkono wako wa kuume hunitegemeza, unajishusha chini ili kuniinua. Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze. Niliwafuatia adui zangu na nikawapata, sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa. Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia BWANA, lakini hakuwajibu. Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo; niliwamwaga nje kama tope barabarani. Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa, watu ambao sikuwajua wananitumikia. Mara wanisikiapo hunitii, wageni hunyenyekea mbele yangu. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, awatiishaye mataifa chini yangu, aniokoaye na adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee BWANA; nitaliimbia sifa jina lako. Humpa mfalme wake ushindi mkuu, huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 18:21-50

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha