Zaburi 18:1-15
Zaburi 18:1-15 BHN
Nakupenda, ee Mwenyezi-Mungu, nguvu yangu! Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa maadui zangu. Kamba za kifo zilinizingira, mawimbi ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake; kilio changu kilimfikia masikioni mwake. Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika; misingi ya milima ikayumbayumba, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake; makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa akaruka; akapaa kasi juu ya mabawa ya upepo. Alijifunika giza pande zote, mawingu mazito yaliyojaa maji yalimzunguka. Umeme ulimulika mbele yake; kukatokea mawinguni mvua ya mawe na makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni; Mungu Mkuu akatoa sauti yake, kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto. Aliwapiga maadui mishale yake, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Ulipowakemea maadui zako ee Mwenyezi-Mungu, ulipowatisha kwa ghadhabu yako, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana.