Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 18:1-15

Zaburi 18:1-15 NEN

Nakupenda wewe, Ee BWANA, nguvu yangu. BWANA ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba, ambaye kwake ninakimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu. Ninamwita BWANA anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea. Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake. Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika. Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake. Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mbawa za upepo. Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka, mawingu meusi ya mvua ya angani. Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikanyesha mvua ya mawe na umeme wa radi. BWANA alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika. Aliipiga mishale yake na kutawanya adui, naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza. Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.