Zab 18:1-15
Zab 18:1-15 SUV
Wewe, BWANA, nguvu zangu, nakupenda sana; BWANA ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo. Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto. BWANA alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto. Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya. Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee BWANA, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.