Zaburi 18:1-15
Zaburi 18:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Nakupenda, ee Mwenyezi-Mungu, nguvu yangu! Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa maadui zangu. Kamba za kifo zilinizingira, mawimbi ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake; kilio changu kilimfikia masikioni mwake. Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika; misingi ya milima ikayumbayumba, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake; makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa akaruka; akapaa kasi juu ya mabawa ya upepo. Alijifunika giza pande zote, mawingu mazito yaliyojaa maji yalimzunguka. Umeme ulimulika mbele yake; kukatokea mawinguni mvua ya mawe na makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni; Mungu Mkuu akatoa sauti yake, kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto. Aliwapiga maadui mishale yake, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Ulipowakemea maadui zako ee Mwenyezi-Mungu, ulipowatisha kwa ghadhabu yako, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana.
Zaburi 18:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wewe, BWANA, nguvu yangu, nakupenda sana; BWANA ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Namwita BWANA astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nilimwita BWANA, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikatingizika; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto wa kuteketeza ukatoka kinywani mwake, Makaa ya moto yakamtoka. Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo. Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Akiwa katika giza la mawingu mazito yaliyojaa maji. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Ikashuka mvua ya mawe na makaa ya moto. BWANA alinguruma kutoka mbinguni, Yeye Aliye Juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto. Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya. Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee BWANA, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.
Zaburi 18:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wewe, BWANA, nguvu zangu, nakupenda sana; BWANA ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo. Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto. BWANA alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto. Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya. Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee BWANA, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.
Zaburi 18:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nakupenda wewe, Ee BWANA, nguvu yangu. BWANA ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba, ambaye kwake ninakimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu. Ninamwita BWANA anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea. Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake. Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika. Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake. Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mbawa za upepo. Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka, mawingu meusi ya mvua ya angani. Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikanyesha mvua ya mawe na umeme wa radi. BWANA alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika. Aliipiga mishale yake na kutawanya adui, naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza. Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.