Methali 23:17-35
Methali 23:17-35 BHN
Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi, ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote. Hakika kuna kesho ya milele, na tumaini lako halitakuwa bure. Sikia mwanangu, uwe na hekima; fikiria sana jinsi unavyoishi. Usiwe mmoja wa walevi wa divai, wala walafi wenye kupenda nyama, maana walevi na walafi wataishia kuwa maskini, anayetumia siku yake kusinzia atavaa matambara. Msikilize baba yako aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako akizeeka. Nunua ukweli, wala usiuuze; nunua hekima, mafunzo na busara. Baba wa mtoto mwadilifu atajaa furaha; anayemzaa mtoto mwenye hekima atamfurahia. Wafurahishe baba na mama yako; mama aliyekuzaa na afurahi. Mwanangu, nisikilize kwa makini, shikilia mwenendo wa maisha yangu. Malaya ni shimo refu la kutega watu; mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba. Yeye hunyemelea kama mnyanganyi, husababisha wanaume wengi kukosa uaminifu. Ni nani wapigao yowe? Ni nani wenye huzuni? Ni nani wenye ugomvi? Ni nani walalamikao? Ni nani wenye majeraha bila sababu? Ni nani wenye macho mekundu? Ni wale ambao hawabanduki penye divai, wale wakaao chonjo kuonja divai iliyokolezwa. Usiitamani divai hata kwa wekundu wake, hata kama inametameta katika bilauri, na kushuka taratibu unapoinywa. Mwishowe huuma kama nyoka; huchoma kama nyoka mwenye sumu. Macho yako yataona mauzauza, moyo wako utatoa mambo yaliyopotoka. Utakuwa kama mtu alalaye katikati ya bahari, kama mtu alalaye juu ya mlingoti wa meli. Utasema, “Walinichapa, lakini sikuumia; walinipiga, lakini sina habari. Nitaamka lini? Ngoja nitafute kinywaji kingine!”