Mithali 23:17-35
Mithali 23:17-35 NENO
Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi, bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Mwenyezi Mungu. Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako, nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali. Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima, weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa. Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa, kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara. Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee. Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu. Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia. Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie! Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu, kwa maana kahaba ni shimo refu na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba. Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia, naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume. Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu? Ni hao wanaokaa sana kwenye mvinyo, hao wanaoenda kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa. Usiukodolee macho mvinyo ukiwa mwekundu, unapometameta kwenye bilauri, unaposhuka taratibu! Mwishowe huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu. Macho yako yataona mambo mageni, na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka. Utakuwa kama alalaye baharini, alalaye juu ya kamba ya merikebu. Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”