Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 23:17-35

Mithali 23:17-35 SRUV

Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi; Bali mche BWANA mchana kutwa; Maana bila shaka iko thawabu; Na tumaini lako halitabatilika. Sikia, mwanangu, uwe na hekima, Na kuuongoza moyo wako katika njia njema. Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa. Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu. Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee. Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu. Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia. Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa. Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu. Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni mtego wa shimo jembamba. Naam, huotea kama mnyang'anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu. Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu? Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika. Usiutazame mvinyo iwapo ni mwekundu; uitiapo bilauri rangi yake, ushukapo taratibu; Mwisho wake huuma kama nyoka; Huchoma kama fira. Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka. Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari; Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti. Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; Wamenipiga wala sina habari; Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena.

Soma Mithali 23