Mathayo 6:5-18
Mathayo 6:5-18 BHN
“Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba. Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: ‘Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo chakula chetu cha kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu.’ [ Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] “Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.