Mathayo 6:5-18
Mathayo 6:5-18 NEN
“Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba. “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni. Utupatie riziki yetu ya kila siku. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu. Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen].’ Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri; naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.