Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:1-13

Luka 22:1-13 BHN

Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda, akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.” Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?” Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. Mwambieni mwenye nyumba: ‘Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.” Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.