Luka 22:1-13
Luka 22:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda, akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.” Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?” Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. Mwambieni mwenye nyumba: ‘Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.” Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
Luka 22:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo sikukuu ya Pasaka. Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskarioti, naye ni mmoja wa wale Kumi na Wawili. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja Pasaka. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akiwa amebeba mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Kiko wapi chumba cha wageni, nipate kula Pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kimekwisha tayarishwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka.
Luka 22:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka. Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.
Luka 22:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu. Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu. Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.” Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?” Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia. Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.” Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.