Lk 22:1-13
Lk 22:1-13 SUV
Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka. Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.