Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:1-13

Luka 22:1-13 NEN

Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu. Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu. Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.” Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?” Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia. Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.” Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.