Yobu 27:13-23
Yobu 27:13-23 BHN
“Hiki ndicho Mungu alichomwekea mtu mwovu, alichopangiwa mdhalimu kupata ni hiki: Watoto wake hata wawe wengi watauawa kwa upanga; wazawa wake hawatakuwa na chakula cha kutosha. Wale watakaopona watakufa kwa maradhi mabaya, na wajane wao hawatawaombolezea. Hata akirundika fedha kama mavumbi, na mavazi kama udongo wa mfinyanzi, na arundike tu, lakini mnyofu ndiye atakayeyavaa, na fedha yake watagawana watu wasio na hatia. Nyumba ajengayo mwovu ni kama utando wa buibui, ni kama kibanda cha mlinzi shambani. Huenda kulala tajiri, lakini ni mara ya mwisho; atafungua macho yake, na utajiri wake umetoweka! Vitisho humvamia kama mafuriko; usiku hukumbwa na kimbunga. Upepo wa mashariki humpeperusha akatoweka; humfagilia mbali kutoka makao yake. Upepo huo humvamia bila huruma; atajaribu kuukimbia lakini mbio za bure. Upepo humzomea akimbiapo, na kumfyonya toka mahali pake.