Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 27:13-23

Ayubu 27:13-23 NEN

“Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu, urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi: Hata kama watoto wake watakuwa wengi kiasi gani, fungu lao ni kuuawa kwa upanga; wazao wake hawatakuwa kamwe na chakula cha kuwatosha. Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao, nao wajane wao hawatawaombolezea. Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi, na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi, yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa, naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake. Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui, kama kibanda alichotengeneza mlinzi. Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho; afunguapo macho yake, yote yametoweka. Vitisho humjia kama mafuriko; dhoruba humkumba ghafula usiku. Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka; humzoa kutoka mahali pake. Humvurumisha bila huruma, huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake. Upepo humpigia makofi kwa dharau, na kumfukuza atoke mahali pake.