Yobu 21:17-34
Yobu 21:17-34 BHN
“Mara ngapi umepata kuona mwanga wa maisha ya mwovu umezimwa, wakapata kukumbwa na maafa, au Mungu amewahi kuwaangamiza kwa hasira yake? Hata hivyo, na wapeperushwe kama majani makavu, wawe kama makapi yanayochukuliwa na dhoruba! “Nyinyi mwasema, ‘Mungu amewawekea watoto wao adhabu ya watu hao waovu.’ Kwa nini hawalipizi wao wenyewe, wapate kutambua! Waone wao wenyewe wakiangamia; waone wenyewe ghadhabu ya Mungu mwenye nguvu. Maana wakifa watajali nini juu ya wazawa wao, wakati siku zao zitakapokuwa zimefika mwisho? Je, binadamu aweza kumfunza Mungu maarifa, Mungu ambaye huwahukumu wakazi wa mbinguni? “Mtu hufa katika kilele cha ufanisi wake, akiwa katika raha mustarehe na salama; amejaa mafuta tele mwilini, na mifupa yake ikiwa bado na nguvu. Mwingine hufa na huzuni kubwa moyoni, akiwa hajawahi kuonja lolote jema. Hata hivyo, wote hufa na kuzikwa, wote hufunikwa na mabuu. “Sikilizeni! Mimi nayajua mawazo yenu yote, na mipango yenu ya kunidharau. Eti mwauliza, ‘Iko wapi nyumba ya mkuu? Iko wapi nyumba alimoishi mwovu?’ “Je, hamjawauliza wapita njia, mkakubaliana na ripoti yao? Mwovu husalimishwa siku ya maafa, huokolewa siku ya ghadhabu! Ni nani atakayemshutumu mtu mwovu, au atakayemlipa kwa yote aliyotenda? Anapochukuliwa kupelekwa kaburini, kaburi lake huwekewa ulinzi. Watu wengi humfuata nyuma na wengine wengi sana humtangulia. Anapozikwa, udongo huteremshwa taratibu. Mtawezaje basi, kunifariji kwa maneno matupu? majibu yenu hayana chochote ila uongo.”