Ayubu 21:17-34
Ayubu 21:17-34 NEN
“Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa? Ni mara ngapi maafa huwajia, yale yawapatayo ambayo Mungu huwapangia katika hasira yake? Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo, kama makapi yachukuliwayo na dhoruba? Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu kwa ajili ya wanawe.’ Mungu na amlipe mtu mwenyewe, ili apate kulijua! Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake; yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi. Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma, miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho? “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa, iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote? Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili, akiwa salama na mwenye raha kamili, mwili wake ukiwa umenawiri, nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake. Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi, akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri. Hao wote hulala mavumbini, nao mabuu huwafunika wote. “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri, mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya. Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu, mahema ambayo watu waovu walikaa?’ Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri? Je, hamkutafakari taarifa zao: kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa, kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu? Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake? Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda? Hupelekwa kaburini, nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake. Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake; watu wote watamfuata, nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia. “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu? Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”