Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 21:17-34

Yobu 21:17-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa? Ni mara ngapi maafa huwajia, yale yawapatayo ambayo Mungu huwapangia katika hasira yake? Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo, kama makapi yachukuliwayo na dhoruba? Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu kwa ajili ya wanawe.’ Mungu na amlipe mtu mwenyewe, ili apate kulijua! Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake; yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi. Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma, miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho? “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa, iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote? Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili, akiwa salama na mwenye raha kamili, mwili wake ukiwa umenawiri, nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake. Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi, akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri. Hao wote hulala mavumbini, nao mabuu huwafunika wote. “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri, mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya. Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu, mahema ambayo watu waovu walikaa?’ Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri? Je, hamkutafakari taarifa zao: kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa, kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu? Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake? Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda? Hupelekwa kaburini, nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake. Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake; watu wote watamfuata, nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia. “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu? Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”

Shirikisha
Soma Yobu 21

Yobu 21:17-34 Biblia Habari Njema (BHN)

“Mara ngapi umepata kuona mwanga wa maisha ya mwovu umezimwa, wakapata kukumbwa na maafa, au Mungu amewahi kuwaangamiza kwa hasira yake? Hata hivyo, na wapeperushwe kama majani makavu, wawe kama makapi yanayochukuliwa na dhoruba! “Nyinyi mwasema, ‘Mungu amewawekea watoto wao adhabu ya watu hao waovu.’ Kwa nini hawalipizi wao wenyewe, wapate kutambua! Waone wao wenyewe wakiangamia; waone wenyewe ghadhabu ya Mungu mwenye nguvu. Maana wakifa watajali nini juu ya wazawa wao, wakati siku zao zitakapokuwa zimefika mwisho? Je, binadamu aweza kumfunza Mungu maarifa, Mungu ambaye huwahukumu wakazi wa mbinguni? “Mtu hufa katika kilele cha ufanisi wake, akiwa katika raha mustarehe na salama; amejaa mafuta tele mwilini, na mifupa yake ikiwa bado na nguvu. Mwingine hufa na huzuni kubwa moyoni, akiwa hajawahi kuonja lolote jema. Hata hivyo, wote hufa na kuzikwa, wote hufunikwa na mabuu. “Sikilizeni! Mimi nayajua mawazo yenu yote, na mipango yenu ya kunidharau. Eti mwauliza, ‘Iko wapi nyumba ya mkuu? Iko wapi nyumba alimoishi mwovu?’ “Je, hamjawauliza wapita njia, mkakubaliana na ripoti yao? Mwovu husalimishwa siku ya maafa, huokolewa siku ya ghadhabu! Ni nani atakayemshutumu mtu mwovu, au atakayemlipa kwa yote aliyotenda? Anapochukuliwa kupelekwa kaburini, kaburi lake huwekewa ulinzi. Watu wengi humfuata nyuma na wengine wengi sana humtangulia. Anapozikwa, udongo huteremshwa taratibu. Mtawezaje basi, kunifariji kwa maneno matupu? majibu yenu hayana chochote ila uongo.”

Shirikisha
Soma Yobu 21

Yobu 21:17-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimwa? Na msiba wao kuwajia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake? Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba? Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua. Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi. Kwani ana furaha gani katika ukoo wake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati? Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu. Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe; Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini. Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe. Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika. Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mipango miovu mnayoazimia kufanya juu yangu. Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu iko wapi? Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui? Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu? Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya? Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya kaburi lake. Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika. Basi imekuwaje ninyi kunituliza moyo kwa utupu mtupu, Kwa kuwa katika majibu yenu unasalia uongo tu.

Shirikisha
Soma Yobu 21

Yobu 21:17-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa? Na msiba wao kuwajilia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake? Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba? Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua. Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi. Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati? Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu. Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe; Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini. Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe. Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika. Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu. Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi? Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui? Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu? Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya? Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya ziara lake. Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika. Basi imekuwaje ninyi kunituza moyo bure, Kwa kuwa katika jawabu zenu unasalia uongo tu.

Shirikisha
Soma Yobu 21