Ayubu 21:17-34
Ayubu 21:17-34 SRUV
Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimwa? Na msiba wao kuwajia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake? Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba? Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua. Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi. Kwani ana furaha gani katika ukoo wake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati? Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu. Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe; Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini. Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe. Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika. Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mipango miovu mnayoazimia kufanya juu yangu. Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu iko wapi? Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui? Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu? Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya? Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya kaburi lake. Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika. Basi imekuwaje ninyi kunituliza moyo kwa utupu mtupu, Kwa kuwa katika majibu yenu unasalia uongo tu.