Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 20:1-11

Yeremia 20:1-11 BHN

Kuhani Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa ofisa mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alimsikia Yeremia akitoa unabii huo. Basi, Pashuri akampiga nabii Yeremia na kumtia kifungoni upande wa lango la juu la Benyamini, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kesho yake asubuhi, Pashuri alipomtoa Yeremia katika mkatale huo, Yeremia alimwambia hivi: “Mwenyezi-Mungu hakuiti tena Pashuri, bali ‘Kitisho Pande Zote’. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Tazama, nitakufanya uwe kitisho kwako wewe mwenyewe na kwa rafiki zako wote. Wao watauawa vitani kwa upanga wa maadui zao huku ukiangalia. Nitawatia watu wote wa Yuda mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atawachukua mateka hadi Babuloni na kuwaua kwa upanga. Zaidi ya hayo, utajiri wote wa mji, mapato yake yote, vitu vyake vyote vya thamani pamoja na hazina zote za wafalme wa Yuda, nitazitia mikononi mwa maadui zao ambao watazipora na kuchukua kila kitu hadi Babuloni. Na kwa upande wako wewe Pashuri, pamoja na nyumba yako yote, mtapelekwa utumwani; hakika mtakwenda Babuloni. Huko ndiko utakakofia na kuzikwa, kadhalika na rafiki zako wote ambao uliwatabiria uongo.’” Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenidanganya, nami kweli nikadanganyika; wewe una nguvu kuliko mimi, nawe umeshinda. Kutwa nzima nimekuwa mtu wa kuchekwa, kila mtu ananidhihaki. Kila ninaposema kitu, nalalamika, napaza sauti, “Ukatili na uharibifu!” Maana kwangu kutangaza neno la Mwenyezi-Mungu kwanifanya nishutumiwe na kudhihakiwa kutwa nzima. Lakini nikisema, “Sitamtaja Mwenyezi-Mungu, wala sitasema tena kwa jina lake,” moyoni mwangu huwa na kitu kama moto uwakao, uliofungiwa ndani ya mifupa yangu. Najaribu sana kuuzuia humo, lakini ninashindwa. Nasikia wengi wakinongona juu yangu. Wananipanga jina: “Kitisho kila upande!” Wengine wanasema: “Nendeni mkamshtaki! Na tumshtaki!” Hata rafiki zangu wote wapenzi wanangojea tu nianguke! Wanasema “Labda atadanganyika, nasi tutalipiza kisasi.” Lakini wewe Mwenyezi-Mungu u pamoja nami kwangu wewe ni kama shujaa wa kutisha; kwa hiyo watesi wangu watajikwaa, na hawataweza kunishinda. Wataaibika kupindukia, maana hawatafaulu. Fedheha yao itakuwa ya daima; kamwe haitasahaulika.

Soma Yeremia 20