Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yer 20:1-11

Yer 20:1-11 SUV

Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya BWANA, alimsikia Yeremia alipokuwa akitabiri maneno hayo. Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya BWANA. Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, BWANA hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu. Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga. Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli. Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo. Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki. Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la BWANA limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia. Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini BWANA yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.

Soma Yer 20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha