Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 20:1-11

Yeremia 20:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya BWANA, alimsikia Yeremia alipokuwa akitoa unabii huo. Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya BWANA. Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, BWANA hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu. Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga. Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli. Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliwatolea unabii wa uongo. Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki. Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la BWANA limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia. Maana nimesikia shutuma za watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini BWANA yuko pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawatafaulu wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.

Shirikisha
Soma Yeremia 20

Yeremia 20:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya BWANA, alimsikia Yeremia alipokuwa akitabiri maneno hayo. Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya BWANA. Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, BWANA hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu. Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga. Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli. Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo. Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki. Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la BWANA limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia. Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini BWANA yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.

Shirikisha
Soma Yeremia 20

Yeremia 20:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ikawa kuhani Pashuri mwana wa Imeri, mkuu wa maafisa wa Hekalu la BWANA, alipomsikia Yeremia akitoa unabii juu ya mambo haya, akaamuru Yeremia nabii apigwe na kufungwa kwenye mkatale katika Lango la Juu la Benyamini huko Hekaluni la BWANA. Siku ya pili Pashuri alipomwachia kutoka kwenye mkatale, Yeremia akamwambia, “BWANA hakukuita jina lako kuwa Pashuri bali Magor-Misabibu. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: ‘Nitakufanya kuwa hofu kuu kwako wewe mwenyewe na rafiki zako wote, na kwa macho yako mwenyewe utawaona wakianguka kwa upanga wa adui zao. Nitawatia Yuda wote mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye atawachukua na kuwapeleka Babeli, ama awaue kwa upanga. Nitatia utajiri wote wa mji huu kwa adui zao: yaani mazao yao yote, vitu vyao vyote vya thamani, na hazina zote za wafalme wa Yuda. Watavitwaa kwa nyara na kuvipeleka Babeli. Nawe Pashuri pamoja na wote waishio katika nyumba yako mtakwenda uhamishoni Babeli. Mtafia humo na kuzikwa, wewe na rafiki zako wote ambao umewatabiria uongo.’ ” Ee BWANA, umenidanganya, nami nikadanganyika; wewe una nguvu kuniliko, nawe umenishinda. Ninadharauliwa mchana kutwa, kila mmoja ananidhihaki. Kila ninenapo, ninapiga kelele nikitangaza ukatili na uharibifu. Kwa hiyo neno la BWANA limeniletea matukano na mashutumu mchana kutwa. Lakini kama nikisema, “Sitamtaja wala kusema tena kwa jina lake,” neno lake linawaka ndani ya moyo wangu kama moto, moto uliofungwa ndani ya mifupa yangu. Nimechoka sana kwa kulizuia ndani mwangu; kweli, siwezi kujizuia. Ninasikia minongʼono mingi, “Hofu iko pande zote! Mshtakini! Twendeni tumshtaki!” Rafiki zangu wote wananisubiri niteleze, wakisema, “Labda atadanganyika; kisha tutamshinda na kulipiza kisasi juu yake.” Lakini BWANA yu pamoja nami kama shujaa mwenye nguvu; hivyo washtaki wangu watajikwaa na kamwe hawatashinda. Watashindwa, nao wataaibika kabisa; kukosa adabu kwao hakutasahauliwa.

Shirikisha
Soma Yeremia 20

Yeremia 20:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Kuhani Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa ofisa mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alimsikia Yeremia akitoa unabii huo. Basi, Pashuri akampiga nabii Yeremia na kumtia kifungoni upande wa lango la juu la Benyamini, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kesho yake asubuhi, Pashuri alipomtoa Yeremia katika mkatale huo, Yeremia alimwambia hivi: “Mwenyezi-Mungu hakuiti tena Pashuri, bali ‘Kitisho Pande Zote’. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Tazama, nitakufanya uwe kitisho kwako wewe mwenyewe na kwa rafiki zako wote. Wao watauawa vitani kwa upanga wa maadui zao huku ukiangalia. Nitawatia watu wote wa Yuda mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atawachukua mateka hadi Babuloni na kuwaua kwa upanga. Zaidi ya hayo, utajiri wote wa mji, mapato yake yote, vitu vyake vyote vya thamani pamoja na hazina zote za wafalme wa Yuda, nitazitia mikononi mwa maadui zao ambao watazipora na kuchukua kila kitu hadi Babuloni. Na kwa upande wako wewe Pashuri, pamoja na nyumba yako yote, mtapelekwa utumwani; hakika mtakwenda Babuloni. Huko ndiko utakakofia na kuzikwa, kadhalika na rafiki zako wote ambao uliwatabiria uongo.’” Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenidanganya, nami kweli nikadanganyika; wewe una nguvu kuliko mimi, nawe umeshinda. Kutwa nzima nimekuwa mtu wa kuchekwa, kila mtu ananidhihaki. Kila ninaposema kitu, nalalamika, napaza sauti, “Ukatili na uharibifu!” Maana kwangu kutangaza neno la Mwenyezi-Mungu kwanifanya nishutumiwe na kudhihakiwa kutwa nzima. Lakini nikisema, “Sitamtaja Mwenyezi-Mungu, wala sitasema tena kwa jina lake,” moyoni mwangu huwa na kitu kama moto uwakao, uliofungiwa ndani ya mifupa yangu. Najaribu sana kuuzuia humo, lakini ninashindwa. Nasikia wengi wakinongona juu yangu. Wananipanga jina: “Kitisho kila upande!” Wengine wanasema: “Nendeni mkamshtaki! Na tumshtaki!” Hata rafiki zangu wote wapenzi wanangojea tu nianguke! Wanasema “Labda atadanganyika, nasi tutalipiza kisasi.” Lakini wewe Mwenyezi-Mungu u pamoja nami kwangu wewe ni kama shujaa wa kutisha; kwa hiyo watesi wangu watajikwaa, na hawataweza kunishinda. Wataaibika kupindukia, maana hawatafaulu. Fedheha yao itakuwa ya daima; kamwe haitasahaulika.

Shirikisha
Soma Yeremia 20