Yeremia 20
20
Ugomvi kati ya Yeremia na Pashuri
1Kuhani Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa ofisa mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alimsikia Yeremia akitoa unabii huo. 2Basi, Pashuri akampiga nabii Yeremia na kumtia kifungoni upande wa lango la juu la Benyamini, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 3Kesho yake asubuhi, Pashuri alipomtoa Yeremia katika mkatale huo, Yeremia alimwambia hivi: “Mwenyezi-Mungu hakuiti tena Pashuri, bali ‘Kitisho Pande Zote’. 4Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Tazama, nitakufanya uwe kitisho kwako wewe mwenyewe na kwa rafiki zako wote. Wao watauawa vitani kwa upanga wa maadui zao huku ukiangalia. Nitawatia watu wote wa Yuda mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atawachukua mateka hadi Babuloni na kuwaua kwa upanga. 5Zaidi ya hayo, utajiri wote wa mji, mapato yake yote, vitu vyake vyote vya thamani pamoja na hazina zote za wafalme wa Yuda, nitazitia mikononi mwa maadui zao ambao watazipora na kuchukua kila kitu hadi Babuloni. 6Na kwa upande wako wewe Pashuri, pamoja na nyumba yako yote, mtapelekwa utumwani; hakika mtakwenda Babuloni. Huko ndiko utakakofia na kuzikwa, kadhalika na rafiki zako wote ambao uliwatabiria uongo.’”
Yeremia anamlalamikia Mungu
7Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenidanganya,
nami kweli nikadanganyika;
wewe una nguvu kuliko mimi,
nawe umeshinda.
Kutwa nzima nimekuwa mtu wa kuchekwa,
kila mtu ananidhihaki.
8Kila ninaposema kitu, nalalamika,
napaza sauti, “Ukatili na uharibifu!”
Maana kwangu kutangaza neno la Mwenyezi-Mungu
kwanifanya nishutumiwe na kudhihakiwa kutwa nzima.
9Lakini nikisema, “Sitamtaja Mwenyezi-Mungu,
wala sitasema tena kwa jina lake,”
moyoni mwangu huwa na kitu kama moto uwakao,
uliofungiwa ndani ya mifupa yangu.
Najaribu sana kuuzuia humo,
lakini ninashindwa.
10Nasikia wengi wakinongona juu yangu.
Wananipanga jina: “Kitisho kila upande!”
Wengine wanasema:
“Nendeni mkamshtaki! Na tumshtaki!”
Hata rafiki zangu wote wapenzi wanangojea tu nianguke!
Wanasema “Labda atadanganyika, nasi tutalipiza kisasi.”
11Lakini wewe Mwenyezi-Mungu u pamoja nami
kwangu wewe ni kama shujaa wa kutisha;
kwa hiyo watesi wangu watajikwaa,
na hawataweza kunishinda.
Wataaibika kupindukia,
maana hawatafaulu.
Fedheha yao itakuwa ya daima;
kamwe haitasahaulika.
12Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
wewe humthibiti mtu mwadilifu,
huona yaliyo moyoni na akilini mwa watu,
unijalie kuona ukiwalipiza kisasi,
maana kwako nimekiweka kisa changu.
13Mwimbieni Mwenyezi-Mungu;
msifuni Mwenyezi-Mungu,
kwani ameyaokoa maisha ya mhitaji,
kutoka mikononi mwa watu waovu.
14Na ilaaniwe siku niliyozaliwa!
Siku hiyo mama aliponizaa,
isitakiwe baraka!
15Na alaaniwe aliyempelekea baba ujumbe:
“Umepata mtoto wa kiume”,
akamfanya ajae furaha.
16Mtu huyo na awe kama miji
aliyoiangusha Mwenyezi-Mungu bila huruma.
Mtu huyo na asikie kilio asubuhi,
na mchana kelele za vita,
17kwani hakuniua tumboni mwa mama yangu;
mama yangu angekuwa kaburi langu,
tumbo lake lingebaki kubwa daima.
18Kwa nini nilitoka tumboni mwa mama yangu?
Je, nilitoka ili nipate taabu na huzuni
na kuishi maisha ya aibu?
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 20: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.