Isaya 21:1-10
Isaya 21:1-10 BHN
Kauli ya Mungu dhidi ya jangwa kando ya bahari. Kama vimbunga vinavyovuma kutoka kusini, wavamizi wanakuja kutoka jangwani, kutoka katika nchi ya kutisha. Nimeoneshwa maono ya kutisha, maono ya watu wa hila watendao hila, maono ya watu waangamizi wafanyao maangamizi. Pandeni juu vitani enyi Waelamu; shambulieni enyi Wamedi! Mungu atakomesha mateso yote yaliyoletwa na Babuloni. Kwa maono hayo nimeingiwa na hofu kubwa, uchungu mwingi umenikumba; kama uchungu wa mama anayejifungua. Maumivu yamenizidi hata siwezi kusikia; nimefadhaika hata siwezi kuona. Moyo unanidunda na woga umenikumba. Nilitamani jioni ifike lakini ilipofika ikawa ya kutetemesha. Chakula kimetayarishwa, shuka zimetandikwa, sasa watu wanakula na kunywa. Ghafla, sauti inasikika: “Inukeni enyi watawala! Wekeni silaha tayari!” Maana Bwana aliniambia, “Nenda ukaweke mlinzi; mwambie atangaze atakachoona. Akiona kikosi, wapandafarasi wawiliwawili, wapandangamia na wapandapunda, na awe macho; naam, akae macho!” Kisha huyo mlinzi akapaza sauti: “Bwana, nimesimama juu ya mnara wa ulinzi mchana kutwa, nimeshika zamu usiku kucha!” Tazama, kikosi kinakuja, wapandafarasi wawiliwawili. Wanasema: “Babuloni umeanguka! Umeanguka! Sanamu zote za miungu yake zimetupwa chini na kuvunjwavunjwa!” Ewe Israeli, watu wangu, enyi mliotwangwa na kupurwa kama nafaka. Sasa nimewaambieni mambo niliyoyasikia kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli.