Isaya 21
21
Maono juu ya kuangamizwa kwa Babuloni
1Kauli ya Mungu dhidi ya jangwa kando ya bahari.#21:1 jangwa kando ya bahari: Pengine Babuloni.
Kama vimbunga vinavyovuma kutoka kusini,
wavamizi wanakuja kutoka jangwani,
kutoka katika nchi ya kutisha.
2Nimeoneshwa maono ya kutisha,
maono ya watu wa hila watendao hila,
maono ya watu waangamizi wafanyao maangamizi.
Pandeni juu vitani enyi Waelamu;
shambulieni enyi Wamedi!
Mungu atakomesha mateso yote
yaliyoletwa na Babuloni.
3Kwa maono hayo nimeingiwa na hofu kubwa,
uchungu mwingi umenikumba;
kama uchungu wa mama anayejifungua.
Maumivu yamenizidi hata siwezi kusikia;
nimefadhaika hata siwezi kuona.
4Moyo unanidunda na woga umenikumba.
Nilitamani jioni ifike
lakini ilipofika ikawa ya kutetemesha.
5Chakula kimetayarishwa,
shuka zimetandikwa,
sasa watu wanakula na kunywa.
Ghafla, sauti inasikika:
“Inukeni enyi watawala!
Wekeni silaha tayari!”
6Maana Bwana aliniambia,
“Nenda ukaweke mlinzi;
mwambie atangaze atakachoona.
7Akiona kikosi, wapandafarasi wawiliwawili,
wapandangamia na wapandapunda,
na awe macho;
naam, akae macho!”
8Kisha huyo mlinzi#21:8 mlinzi: Kwa kubadili konsonanti na kupatana na hati ya Kumrani na tafsiri ya Peshita. Kiebrania: Simba. akapaza sauti:
“Bwana, nimesimama juu ya mnara wa ulinzi mchana kutwa,
nimeshika zamu usiku kucha!”
9 #21:9 Taz Ufu 14:8; 18:2. Tazama, kikosi kinakuja,
wapandafarasi wawiliwawili.
Wanasema: “Babuloni umeanguka! Umeanguka!
Sanamu zote za miungu yake
zimetupwa chini na kuvunjwavunjwa!”
10Ewe Israeli, watu wangu,
enyi mliotwangwa na kupurwa kama nafaka.
Sasa nimewaambieni mambo niliyoyasikia
kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli.
Ufunuo kuhusu Edomu
11Kauli ya Mungu dhidi ya Duma.
Ninasikia mtu ananiita kutoka Seiri:
“Mlinzi, nini kipya leo usiku?
Kuna kipya chochote leo usiku?”
12Nami mlinzi nikajibu:
“Asubuhi inakuja, kadhalika na usiku;
ukitaka kuuliza, uliza tu;
nenda urudi tena.”
Ufunuo kuhusu Arabia
13Kauli ya Mungu dhidi ya Arabia.
Enyi misafara ya Dedani,
pigeni kambi leo usiku kwenye nyika za Arabia.
14Enyi wakazi wa nchi ya Tema,
wapeni maji hao wenye kiu;
wapelekeeni chakula hao wakimbizi.
15Maana wamekimbia mapanga,
mapanga yaliyochomolewa,
pinde zilizovutwa na ukali wa mapigano.
16Maana Bwana aliniambia hivi: “Katika muda wa mwaka mmoja, bila kuzidi wala kupungua, fahari yote ya Kedari itakwisha. 17Wapiga upinde wachache kati ya mashujaa wa watu wa Kedari ndio watakaosalia. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.”
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 21: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.