Isaya 21:1-10
Isaya 21:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Kauli ya Mungu dhidi ya jangwa kando ya bahari. Kama vimbunga vinavyovuma kutoka kusini, wavamizi wanakuja kutoka jangwani, kutoka katika nchi ya kutisha. Nimeoneshwa maono ya kutisha, maono ya watu wa hila watendao hila, maono ya watu waangamizi wafanyao maangamizi. Pandeni juu vitani enyi Waelamu; shambulieni enyi Wamedi! Mungu atakomesha mateso yote yaliyoletwa na Babuloni. Kwa maono hayo nimeingiwa na hofu kubwa, uchungu mwingi umenikumba; kama uchungu wa mama anayejifungua. Maumivu yamenizidi hata siwezi kusikia; nimefadhaika hata siwezi kuona. Moyo unanidunda na woga umenikumba. Nilitamani jioni ifike lakini ilipofika ikawa ya kutetemesha. Chakula kimetayarishwa, shuka zimetandikwa, sasa watu wanakula na kunywa. Ghafla, sauti inasikika: “Inukeni enyi watawala! Wekeni silaha tayari!” Maana Bwana aliniambia, “Nenda ukaweke mlinzi; mwambie atangaze atakachoona. Akiona kikosi, wapandafarasi wawiliwawili, wapandangamia na wapandapunda, na awe macho; naam, akae macho!” Kisha huyo mlinzi akapaza sauti: “Bwana, nimesimama juu ya mnara wa ulinzi mchana kutwa, nimeshika zamu usiku kucha!” Tazama, kikosi kinakuja, wapandafarasi wawiliwawili. Wanasema: “Babuloni umeanguka! Umeanguka! Sanamu zote za miungu yake zimetupwa chini na kuvunjwavunjwa!” Ewe Israeli, watu wangu, enyi mliotwangwa na kupurwa kama nafaka. Sasa nimewaambieni mambo niliyoyasikia kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli.
Isaya 21:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo juu ya nyika kando ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka kwa nyika, toka nchi itishayo. Nimeoneshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote. Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, uchungu umenishika, kama uchungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapigapiga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha. Wanaandaa meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta. Maana Bwana ameniambia hivi, Nenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze. Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; na asikilize kwa makini, kwa makini sana. Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini. Ewe wangu niliyekufikicha na kukupura; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nayatangaza kwenu.
Isaya 21:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo juu ya bara ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka bara, toka nchi itishayo. Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote. Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha. Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta. Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze. Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza. Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini. Ewe niliyekufikicha, na nafaka ya sakafu yangu; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nimewapasha habari zake.
Isaya 21:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari: Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini, mshambuliaji anakuja kutoka jangwani, kutoka nchi inayotisha. Nimeonyeshwa maono ya kutisha: Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara. Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi! Nitakomesha huzuni zote alizosababisha. Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu, maumivu makali ya ghafula yamenishika, kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa. Nimeduwazwa na lile ninalolisikia, nimeshangazwa na lile ninaloliona. Moyo wangu unababaika, woga unanifanya nitetemeke, gizagiza la jioni nililolitamani sana, limekuwa hofu kuu kwangu. Wanaandaa meza, wanatandaza mazulia, wanakula, wanakunywa! Amkeni, enyi maafisa, zitieni ngao mafuta! Hili ndilo Bwana analoniambia: “Nenda, weka mlinzi, na atoe taarifa ya kile anachokiona. Anapoona magari ya vita pamoja na kundi la farasi, wapanda punda au wapanda ngamia, na awe macho, awe macho kikamilifu.” Naye mlinzi alipaza sauti, “Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi, kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa. Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita pamoja na kundi la farasi. Naye anajibu: ‘Babeli umeanguka, umeanguka! Vinyago vyote vya miungu yake vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ” Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria, ninawaambia kile nilichokisikia kutoka kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote, kutoka kwa Mungu wa Israeli.