Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 21:1-10

Isaya 21:1-10 NEN

Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari: Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini, mshambuliaji anakuja kutoka jangwani, kutoka nchi inayotisha. Nimeonyeshwa maono ya kutisha: Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara. Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi! Nitakomesha huzuni zote alizosababisha. Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu, maumivu makali ya ghafula yamenishika, kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa. Nimeduwazwa na lile ninalolisikia, nimeshangazwa na lile ninaloliona. Moyo wangu unababaika, woga unanifanya nitetemeke, gizagiza la jioni nililolitamani sana, limekuwa hofu kuu kwangu. Wanaandaa meza, wanatandaza mazulia, wanakula, wanakunywa! Amkeni, enyi maafisa, zitieni ngao mafuta! Hili ndilo Bwana analoniambia: “Nenda, weka mlinzi, na atoe taarifa ya kile anachokiona. Anapoona magari ya vita pamoja na kundi la farasi, wapanda punda au wapanda ngamia, na awe macho, awe macho kikamilifu.” Naye mlinzi alipaza sauti, “Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi, kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa. Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita pamoja na kundi la farasi. Naye anajibu: ‘Babeli umeanguka, umeanguka! Vinyago vyote vya miungu yake vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ” Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria, ninawaambia kile nilichokisikia kutoka kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote, kutoka kwa Mungu wa Israeli.