Ezekieli 32:1-16
Ezekieli 32:1-16 BHN
Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa kumi na mbili tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Imba utenzi wa kuomboleza juu ya Farao, mfalme wa Misri. Wewe Farao unajiona kuwa simba kati ya mataifa, lakini wewe ni kama mamba tu majini: Unachomoka kwa nguvu kwenye mito yako, wayavuruga maji kwa miguu yako, na kuichafua mito. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitautupa wavu wangu juu yako, nao watu watakuvua humo kwa wavu wangu. Nitakutupa juu ya nchi kavu, nitakubwaga uwanjani, nitawafanya ndege wote watue juu yako, na kuwashibisha wanyama wote wa porini kwa mwili wako. Nitatawanya nyama yako milimani, na kujaza mabonde yote mzoga wako. Nchi nitainywesha damu yako mpaka milimani, mashimo yatajaa damu yako. Nitakapokuangamiza, nitazifunika mbingu, nitazifanya nyota kuwa nyeusi, jua nitalifunika kwa mawingu, na mwezi hautatoa mwangaza wake. Nitaifanya mianga yote mbinguni kuwa giza, nitatandaza giza juu ya nchi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitaihuzunisha mioyo ya watu wengi, nitakapokupeleka utumwani kati ya mataifa, katika nchi ambazo huzijua. Nitayashtusha mataifa mengi kwa habari zako, wafalme wao watatetemeka kwa sababu yako, nitakaponyosha upanga wangu mbele yao. Watatetemeka kila wakati, kila mtu akihofia uhai wake, siku ile ya kuangamia kwako. Kwa maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Upanga wa mfalme wa Babuloni utakufuatia. Watu wako wengi watauawa kwa mapanga ya mashujaa, watu katili kuliko mataifa yote. Watakomesha kiburi cha Misri na kuwaua watu wako wote. Nitaiangamiza mifugo yako yote kando ya mto Nili. Maji yake hayatavurugwa tena na mtu wala kwato za mnyama kuyachafua tena. Hapo nitayafanya maji yake yatulie na kuitiririsha mito yake kama mafuta. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na mali yake yote kuchukuliwa, nitakapowaua wakazi wake wote, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Huo ndio utenzi wa maombolezo, wanawake wa mataifa watauimba, wataimba juu ya Misri na watu wake wote. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”