Ezekieli 32:1-16
Ezekieli 32:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa kumi na mbili tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Imba utenzi wa kuomboleza juu ya Farao, mfalme wa Misri. Wewe Farao unajiona kuwa simba kati ya mataifa, lakini wewe ni kama mamba tu majini: Unachomoka kwa nguvu kwenye mito yako, wayavuruga maji kwa miguu yako, na kuichafua mito. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitautupa wavu wangu juu yako, nao watu watakuvua humo kwa wavu wangu. Nitakutupa juu ya nchi kavu, nitakubwaga uwanjani, nitawafanya ndege wote watue juu yako, na kuwashibisha wanyama wote wa porini kwa mwili wako. Nitatawanya nyama yako milimani, na kujaza mabonde yote mzoga wako. Nchi nitainywesha damu yako mpaka milimani, mashimo yatajaa damu yako. Nitakapokuangamiza, nitazifunika mbingu, nitazifanya nyota kuwa nyeusi, jua nitalifunika kwa mawingu, na mwezi hautatoa mwangaza wake. Nitaifanya mianga yote mbinguni kuwa giza, nitatandaza giza juu ya nchi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitaihuzunisha mioyo ya watu wengi, nitakapokupeleka utumwani kati ya mataifa, katika nchi ambazo huzijua. Nitayashtusha mataifa mengi kwa habari zako, wafalme wao watatetemeka kwa sababu yako, nitakaponyosha upanga wangu mbele yao. Watatetemeka kila wakati, kila mtu akihofia uhai wake, siku ile ya kuangamia kwako. Kwa maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Upanga wa mfalme wa Babuloni utakufuatia. Watu wako wengi watauawa kwa mapanga ya mashujaa, watu katili kuliko mataifa yote. Watakomesha kiburi cha Misri na kuwaua watu wako wote. Nitaiangamiza mifugo yako yote kando ya mto Nili. Maji yake hayatavurugwa tena na mtu wala kwato za mnyama kuyachafua tena. Hapo nitayafanya maji yake yatulie na kuitiririsha mito yake kama mafuta. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na mali yake yote kuchukuliwa, nitakapowaua wakazi wake wote, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Huo ndio utenzi wa maombolezo, wanawake wa mataifa watauimba, wataimba juu ya Misri na watu wake wote. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Ezekieli 32:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwanasimba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao. Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu. Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe. Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako. Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe. Nami nitakapokuzimisha, nitazifunika mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU. Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua. Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujia. Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako umati wote; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia. Tena nitawaangaza mifugo wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua. Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU. Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Hayo ndiyo maombolezo watakayoimba; binti za mataifa watayaimba; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake umati wote, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 32:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwana-simba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao. Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu. Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe. Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako. Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe. Nami nitakapokuzimisha, nitazifunikiza mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU. Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua. Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujilia. Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako wote jamii; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia. Tena nitawaharibu wanyama wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua. Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU. Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 32:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie: “ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa, wewe ni kama joka kubwa baharini, unayevuruga maji kwa miguu yako na kuchafua vijito. “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu nitautupa wavu wangu juu yako, nao watakukokota katika wavu wangu. Nitakutupa nchi kavu na kukuvurumisha uwanjani. Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako na wanyama wote wa nchi watajishibisha nyama yako. Nitatawanya nyama yako juu ya milima na kujaza mabonde kwa mabaki yako. Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka njia yote hadi milimani, nayo mabonde yatajazwa na nyama yako. Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu na kuzitia nyota zake giza; nitalifunika jua kwa wingu, nao mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote itoayo nuru angani nitaitia giza juu yako; nitaleta giza juu ya nchi yako, asema BWANA Mwenyezi. Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa, nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi ambazo haujapata kuzijua. Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie, wafalme wao watatetemeka kwa hofu kwa ajili yako nitakapotikisa upanga wangu mbele yao. Siku ya anguko lako kila mmoja wao atatetemeka kila dakika kwa ajili ya maisha yake. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli utakuja dhidi yako. Nitafanya makundi yako ya wajeuri kuanguka kwa panga za watu mashujaa, taifa katili kuliko mataifa yote. Watakivunjavunja kiburi cha Misri, nayo makundi yake yote ya wajeuri yatashindwa. Nitaangamiza mifugo yake yote wanaojilisha kando ya maji mengi, hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu wala kwato za mnyama hazitayachafua tena. Kisha nitafanya maji yake yatulie na kufanya vijito vyake vitiririke kama mafuta, asema BWANA Mwenyezi. Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa na kuiondolea nchi kila kitu kilichomo ndani yake, nitakapowapiga wote waishio humo, ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote ya wajeuri wataliimba, asema BWANA Mwenyezi.”