Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 32:1-16

Ezekieli 32:1-16 NEN

Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie: “ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa, wewe ni kama joka kubwa baharini, unayevuruga maji kwa miguu yako na kuchafua vijito. “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu nitautupa wavu wangu juu yako, nao watakukokota katika wavu wangu. Nitakutupa nchi kavu na kukuvurumisha uwanjani. Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako na wanyama wote wa nchi watajishibisha nyama yako. Nitatawanya nyama yako juu ya milima na kujaza mabonde kwa mabaki yako. Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka njia yote hadi milimani, nayo mabonde yatajazwa na nyama yako. Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu na kuzitia nyota zake giza; nitalifunika jua kwa wingu, nao mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote itoayo nuru angani nitaitia giza juu yako; nitaleta giza juu ya nchi yako, asema BWANA Mwenyezi. Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa, nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi ambazo haujapata kuzijua. Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie, wafalme wao watatetemeka kwa hofu kwa ajili yako nitakapotikisa upanga wangu mbele yao. Siku ya anguko lako kila mmoja wao atatetemeka kila dakika kwa ajili ya maisha yake. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli utakuja dhidi yako. Nitafanya makundi yako ya wajeuri kuanguka kwa panga za watu mashujaa, taifa katili kuliko mataifa yote. Watakivunjavunja kiburi cha Misri, nayo makundi yake yote ya wajeuri yatashindwa. Nitaangamiza mifugo yake yote wanaojilisha kando ya maji mengi, hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu wala kwato za mnyama hazitayachafua tena. Kisha nitafanya maji yake yatulie na kufanya vijito vyake vitiririke kama mafuta, asema BWANA Mwenyezi. Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa na kuiondolea nchi kila kitu kilichomo ndani yake, nitakapowapiga wote waishio humo, ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote ya wajeuri wataliimba, asema BWANA Mwenyezi.”