Eze 32:1-16
Eze 32:1-16 SUV
Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwana-simba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao. Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu. Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe. Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako. Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe. Nami nitakapokuzimisha, nitazifunikiza mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU. Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua. Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujilia. Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako wote jamii; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia. Tena nitawaharibu wanyama wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua. Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU. Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.