Ezekieli 23:22-35
Ezekieli 23:22-35 BHN
“Sasa Oholiba! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawafanya wapenzi wako uliowaacha kwa chuki wainuke dhidi yako; nitawaleta wakushambulie kutoka pande zote. Nitawachochea Wababuloni na Wakaldayo wote, watu toka Pekodi, Shoa na Koa, pamoja na Waashuru wote. Nitawachochea vijana wote wa kuvutia, wakuu wa mikoa, makamanda, maofisa na wanajeshi wote wakiwa wapandafarasi. Watakujia kutoka kaskazini, pamoja na magari ya vita na ya mizigo, wakiongoza kundi kubwa la watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao kubwa na ndogo na kofia za chuma. Nimewapa uwezo wa kukuhukumu, nao watakuhukumu kadiri ya sheria zao. Nami nitakuelekezea ghadhabu yangu, nao watakutenda kwa hasira kali. Watakukata pua na masikio na watu wako watakaosalia watauawa kwa upanga. Watawachukua watoto wako wa kiume na wa kike, na watu wako watakaosalia watateketezwa kwa moto. Watakuvua mavazi yako na kukunyanganya johari zako nzuri. Nitaukomesha uasherati na uzinzi wako ulioufanya tangu ulipokuwa kule Misri. Hutaziangalia sanamu zozote tena wala kuifikiria tena nchi ya Misri. “Naam, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakutia mikononi mwa watu unaowachukia, watu unaowaona kuwa kinyaa. Na, kwa vile wanakuchukia, watakunyanganya matunda yote ya kazi yako na kukuacha uchi, bila nguo na kuonesha aibu ya uzinzi wako. Uzinzi wako na uasherati wako ndivyo vilivyokuletea hali hiyo. Wewe ulizini na mataifa, ukajitia najisi kwa miungu yao. Kwa kuwa ulifuata nyayo za dada yako, basi, mimi nitakupa kikombe kilekile cha adhabu ukinywe. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Utakunywa toka kikombe cha dada yako; kikombe kikubwa na cha kina kirefu. Watu watakucheka na kukudharau; na kikombe chenyewe kimejaa. Kitakulewesha na kukuhuzunisha sana. Kikombe cha dada yako Samaria, ni kikombe cha hofu na maangamizi. Utakinywa na kukimaliza kabisa; utakipasua vipandevipande kwa meno, na kurarua navyo matiti yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa umenisahau na kunipa kisogo, basi, utawajibika kwa uasherati na uzinzi wako.”