Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:22-35

Ezekieli 23:22-35 Biblia Habari Njema (BHN)

“Sasa Oholiba! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawafanya wapenzi wako uliowaacha kwa chuki wainuke dhidi yako; nitawaleta wakushambulie kutoka pande zote. Nitawachochea Wababuloni na Wakaldayo wote, watu toka Pekodi, Shoa na Koa, pamoja na Waashuru wote. Nitawachochea vijana wote wa kuvutia, wakuu wa mikoa, makamanda, maofisa na wanajeshi wote wakiwa wapandafarasi. Watakujia kutoka kaskazini, pamoja na magari ya vita na ya mizigo, wakiongoza kundi kubwa la watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao kubwa na ndogo na kofia za chuma. Nimewapa uwezo wa kukuhukumu, nao watakuhukumu kadiri ya sheria zao. Nami nitakuelekezea ghadhabu yangu, nao watakutenda kwa hasira kali. Watakukata pua na masikio na watu wako watakaosalia watauawa kwa upanga. Watawachukua watoto wako wa kiume na wa kike, na watu wako watakaosalia watateketezwa kwa moto. Watakuvua mavazi yako na kukunyanganya johari zako nzuri. Nitaukomesha uasherati na uzinzi wako ulioufanya tangu ulipokuwa kule Misri. Hutaziangalia sanamu zozote tena wala kuifikiria tena nchi ya Misri. “Naam, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakutia mikononi mwa watu unaowachukia, watu unaowaona kuwa kinyaa. Na, kwa vile wanakuchukia, watakunyanganya matunda yote ya kazi yako na kukuacha uchi, bila nguo na kuonesha aibu ya uzinzi wako. Uzinzi wako na uasherati wako ndivyo vilivyokuletea hali hiyo. Wewe ulizini na mataifa, ukajitia najisi kwa miungu yao. Kwa kuwa ulifuata nyayo za dada yako, basi, mimi nitakupa kikombe kilekile cha adhabu ukinywe. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Utakunywa toka kikombe cha dada yako; kikombe kikubwa na cha kina kirefu. Watu watakucheka na kukudharau; na kikombe chenyewe kimejaa. Kitakulewesha na kukuhuzunisha sana. Kikombe cha dada yako Samaria, ni kikombe cha hofu na maangamizi. Utakinywa na kukimaliza kabisa; utakipasua vipandevipande kwa meno, na kurarua navyo matiti yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa umenisahau na kunipa kisogo, basi, utawajibika kwa uasherati na uzinzi wako.”

Ezekieli 23:22-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawachochea wapenzi wako juu yako, hao ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote; watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, watawala na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi. Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu kulingana na hukumu zao. Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni. Pia watakuvua nguo zako, na kukunyang'anya johari zako uzuri. Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena. Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao; nao watakutenda mambo kwa chuki, watakunyang'anya matunda yote ya kazi yako, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao. Umekwenda katika njia ya dada yako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako. Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha dada yako; chenye kina kirefu na kipana; utadhihakiwa na kudharauliwa; nacho kimejaa sana. Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria. Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.

Ezekieli 23:22-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainua wapenzi wako juu yako, ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote; watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi. Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu sawasawa na hukumu zao. Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa, upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni. Pia watakuvua nguo zako, na kukuondolea vyombo vyako vya uzuri. Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena. Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao; nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao. Umekwenda katika njia ya umbu lako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako. Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha umbu lako; chenye nafasi nyingi kikubwa; utadhihakiwa na kudharauliwa; kimejaa sana. Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha umbu lako Samaria. Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.

Ezekieli 23:22-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande: Wababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi. Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kofia za chuma. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao. Nitaelekeza wivu wa hasira yangu dhidi yako, nao watakushughulikia kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako na binti zako, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto. Watakuvua pia nguo zako na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu. Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani tena, wala kukumbuka Misri tena. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia. Watakushughulikia kwa chuki na kukunyangʼanya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako, kikombe kikubwa na chenye kina kirefu; nitaletea juu yako dharau na dhihaka, kwa kuwa kimejaa sana. Utalewa ulevi na kujawa huzuni, kikombe cha maangamizo na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria. Utakinywa chote na kukimaliza; utakivunja vipande vipande na kuyararua matiti yako. Nimenena haya, asema BWANA Mwenyezi. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”