Ezekieli 23:22-35
Ezekieli 23:22-35 SRUV
Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawachochea wapenzi wako juu yako, hao ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote; watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, watawala na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi. Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu kulingana na hukumu zao. Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni. Pia watakuvua nguo zako, na kukunyang'anya johari zako uzuri. Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena. Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao; nao watakutenda mambo kwa chuki, watakunyang'anya matunda yote ya kazi yako, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao. Umekwenda katika njia ya dada yako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako. Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha dada yako; chenye kina kirefu na kipana; utadhihakiwa na kudharauliwa; nacho kimejaa sana. Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria. Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.